Sunday, September 26, 2010

Serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi ya 2005 kwa mafanikio makubwa.

Na Mwandishi Maalumu, Lindi
MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewataka wanachama wa CCM kutembea kifua mbele kwa sababu serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi ya 2005 kwa mafanikio makubwa.Alisema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti jana na juzi na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika majimbo ya Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini, Mchinga, Mtama, Lindi Mjini, Ruangwa na Nachingwea.Mwenyekiti huyo alisema kama yalivyo maeneo mengine nchini, ndivyo ilivyo katika majimbo hayo kwa maendeleo yaliyopatikana katika miaka mitano ya serikali ya awamu ya nne hali inayodhihirisha utekelezaji mzuri wa ilani hiyo.“Hivi mtu anapotoka huko na kusema CCM haijafanya lolote, alitaka ifanye nini? Wana-CCM tembeeni kwa kujidai kwa sababu katika kipindi cha miaka mitano serikali imefanya mambo mengi mazuri kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema na kupigiwa kofi.Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2005 katika majimbo hayo ilitaja baadhi ya maendeleo yaliyopatikana ni kuongezeka kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, kuboreka kwa barabara, huduma ya maji na kina mama kuwa na mwamko wa kujishughulisha na miradi inayowaingizia pesa.Mfano, katika wilaya ya Kilwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wamefikia 6,300 ikilinganishwa na 1,280 wa mwaka 2005, shule za sekondari zilikuwa nne kwa sasa ziko 25 huku idadi ya walimu ikiongezeka kutoka 35 na kufikia 128.Wilaya ya Kilwa kwa miaka mingi ilikuwa na tatizo sugu la upatikanaji wa umeme lakini kwa sasa shida hiyo ni historia baada ya kuwa na umeme wa uhakika unaotokana na gesi ya Songosongo.Mama Salma alisema, kwa mafanikio hayo ni wazi CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi, na kuwataka kina mama kutopoteza kura zao kwa kukivipigia kura vyama vya upinzani ambavyo haviwezi kushinda katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.Aliwataka wazazi kuwasimamia watoto wao wasome kwa bidiii kwa sababu elimu ndiyo msingi mkuu wa maendeleo kwa nchi yoyote.“Mtu asikudanganye, nchi zote zilizopiga hatua katika maendeleo zimewekeza katika elimu kwa vijana wao, na ndicho serikali imekifanya katika miaka mitano hii,” alisema.Alisema baada ya ujenzi wa shule za sekondari za kata kutia for a, ni dhamira ya Chama Cha Mapinduzi kuona wanaomaliza kidato cha nne wanaendelea kupata elimu ya kidato cha tano na sita, hivyo kila tarafa itajengwa shule yenye vidato hivyo.Alikemea tabia ya undumila inayoonyeshwa na baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM, akisema isipoachwa itakikosesha ushindi wa kishindo katika uchaguzi.“Wengine hapa mchana wamevaa kijani, usiku wako kwenye vyama vingine, kweli au si kweli,” alihoji Mama Salma na kujibiwa kwa sauti “kweli, sema mama.” Aliwasihi viongozi na wanachama waondoe tofauti miongoni mwao na kuwa kitu kimoja kuwezesha ushindi mkubwa kwa CCM, kwani kuendelea na hali ya kutofautiana ni kutoa upenyo kwa wapinzani.





No comments:

Post a Comment