Monday, September 13, 2010

Mama Salma apongezwa kusaidia wanawake

 NA MWANDISHI MAALUMU, MUSOMA
WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Mara, wamempongeza Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, kwa jitihada zake za kushughulikia kero zinazowakabili wanawake pasipo kujali itikadi.Katika taarifa za utendaji kazi zilizowasilishwa kwake Septemba 13,2010, na makatibu wa UWT wa wilaya za Musoma Mjini, Musoma Vijijini na Bunda, mkoani humo, zilieleza kwamba Mama Salma amewasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi pamoja na kupigania elimu kwa watoto wa kike. Makatibu hao, Agness Methew (Bunda), Ashura Kimwaga (Musoma Mjini) na Hamisa Chacha (Musoma Vijijini), kwa nyakati tofauti walisema kwamba bila kujali itikadi amekuwa akiwawezesha kiuchumi kina mama katika vikundi vyao vya uzalishaji mali.
 Watendaji hao wa UWT walimsifu Mama Salma kwa kuwa mstari wa mbele kupigania elimu kwa watoto wa kike, jambo ambalo ni ukombozi katika maisha yao ya baadaye.Mama Salma ambaye yuko mkoani Mara kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu, na kuwapigia kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi, alisema kwamba, Ilani ya CCM ya 2005 ilizungumza kuwawezesha kina mama kiuchumi, na kuwapatia nafasi katika vyombo vya maamuzi, mambo ambayo yametekelezwa kwa kiwango kikubwa.Alifafanua kwamba uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake umefanyika kupitia vyama vya ushirika (SACCOS) hatua ambayo imewapa uwezo wa kumudu gharama za mahitaji yao na ya familia zao.Mama Salma aliwakumbusha kina mama hao kwamba, kwa kuwa fedha zinazotolewa kupitia SACCOS ni mikopo, ni muhimu kwa kila anayezikopa kuzirejesha kwa wakati kuwezesha wengine kutumia fursa hiyo na kujikwamua kiuchumi. “Licha ya wanawake kuwezeshwa kiuchumi katika kipindi hiki cha miaka mitano, pia wengi wapo katika ngazi za maamuzi,” alisema.Mama Salma aliwataka wanachama wa CCM kuyatangaza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2005 pasipo woga, kwa sababu mengi yaliyoahidiwa yametekelezwa kwa asilimia kubwa.Alifafanua kwamba, katika harakati za kuleta maendeleo, changamoto haziwezi kukosekana na kutoa mfano kwamba, mafanikio katika ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata nchini, yameibua upungufu wa walimu, maabara na nyumba za kuishi watumishi hao.Mama Salma alisema serikali inazifahamu changamoto hizo, na ndiyo msingi wa kuongeza bajeti ya elimu kuwezesha kutatuliwa na kuwepo kwa wanafunzi wengi wanaosomea ualimu katika vyuo mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo katika chuo chake cha ualimu, kila mwaka kitakuwa kikitoa wahitimu wa ualimu 15,000 hatua ambayo itaoondoa tatizo la watumishi hao nchini kote katika kipindi kifupi kijacho.Aliwasihi Watanzania wasidanganyike na kauli za wapinzani kwamba watakapoingia madarakani kila kitu kitakuwa bure, na hawatatoza kodi.“Hakuna serikali yoyote hapa duniani inayoendeshwa pasipo kutoza kodi. Tusidanganyike,” alisema na kuitikiwa; “hatutadanganyiki.” Mama Salma aliwanadi wagombea ubunge kupitia CCM, Stephen Wassira (Bunda) na Vedastus Mathayo (Musoma Mjini). Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono amepita bila kupingwa.Tayari Mama Salma ameshafanya ziara kama hiyo na kuzungumza na kina mama kwenye mikutano ya ndani, katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Singida, Manyara na Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment