Na Mwaandishi Maalum,Mtwara:
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amekifananisha Chama Cha Mapinduzi na mwembe ambao hurushiwa mawe kutokana na matunda yake. Alisema wapinzani wanaisema CCM kwa sababu serikali imefanya mambo mazuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa baada ya kutekeleza kwa mafanikio ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya 2005. “Ukiona wapinzani wanaisema sana CCM ujue imefanya mambo mazuri, ni sawa na mwembe wenye matunda hupigwa mawe, kwani umeshaona mwembe usio na matunda ukipigwa mawe,” alihoji. Mama Salma alisema hayo jana na juzi alipokuwa akizungumza kwa wakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika mkoa wa Mtwara. Kuhusu uchumi, aliwaambia uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni ukombozi kwa wakulima dhidi ya walanguzi. Taarifa iliyowasilishwa kwake ilieleza kwamba, uuzaji korosho kwa mfumo huo umewanufaisha wakulima ambao hulipwa malipo kwa awamu mbili hadi tatu kulingana na bei ya soko. Ilieleza kwamba, wakati serikali ya awamu ya nne inaiingia madarakani kilo moja ya korosho ilikuwa ikiuzwa kwa kati ya sh. 150 hadi 300, kwa sasa ni sh. 800 hadi sh.1000 kwa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani. Mama Salma alisema wanaoupinga mfumo huo, wanataka kuendelea kujitajirisha kwa jasho la wakulima kama ilivyokuwa huko nyuma. “Msidanayike, uuzaji wa mazao kwa stakakabadhi ya mazao ghalani ni ukombozi kwa wakulima, na serikali ya CCM inawapenda haiwezi kuwadhulumu ndiyo maana inasisitiza na kusimamia mazao kuuzwa kwa vyama vya ushirika,” alisema na kupigiwa kofi na vigelegele. Wakati akiwanadi wagombea ubunge Mariam Kasembe (Masasi), Jerome Bwanausi (Lulindi), George Mkuchika (Newala), Juma Njwayo (Tandahimba), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) na Mohamed Murji (Mtwara Mjini), Mama Salma alitoa wito kwa wanawake viongozi kupigania kwa dhati maendeleo ya kina mama wenzao. Alisema haipendezi mwanamke kiongozi kuwa kikwazo katika maendeleo ya wenzake, alibainisha Mama Salma na kushangiliwa na kina mama hao.
No comments:
Post a Comment