Friday, September 17, 2010

Wito kwa wagombea waliokosa wapinzani

NA MWANDISHI MAALUMU, KONGWA
 MWENYEKITI  wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao katika kata na majimbo yao wagombea wamepita bila kupingwa, wasibweteke, waendelee kufanya kampeni za nguvu kukiwezesha chama kupata  ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31, mwaka huu.Mama Salma alisema hayo Agosti 29, 2010,  alipozungumza na wanawake wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo.Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaomba kinamama hao kuwachagua wagombea wa CCM kwa mtindo maarufu wa chama hicho wa mafiga matatu, yaani diwani, mbunge na rais.Taarifa ya chama hicho wilayani Kongwa, ilieleza kwamba mbunge anayetetea nafasi yake katika jimbo la Kongwa, Job Ndugai wa CCM, amekosa mpinzani, na wagombea udiwani nane kati ya 22 nao wamepita bila kupingwa.Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa Kongwa kwa zaidi ya asilimia 85, ambapo kwa upande wa shule za sekondari zimeoongezeka kutoka tano mwaka 2005 hadi kufikia 24, huku baadhi ya kata zikiwa na shule tatu za sekondari kulingana na idadi ya wanafunzi wa maeneo husika.Kutokana na ongezeko la shule hiyo, taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Kongwa, Abdi Matali, ilisema wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari nao wameongezeka kutoka 1,324 mwaka 2005 hadi kufikia 9,850.Mama Salma alisema kwamba, CCM ina kila sababu ya kuchaguliwa kuendelea kushika dola kwa sababu imetekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 iliyonadiwa nchini kote na kukubaliwa na wananchi.

No comments:

Post a Comment