Sunday, September 12, 2010

Zingatieni masharti mikopo isaidie wengi

NA MWANDISHI MAALUM, RUFIJI
WANAWAKE wanaokopa kutoka taasisi za fedha, wamekumbushwa kuzingatia masharti ya mikopo ikiwa ni pamoja na kuirejesha kwa wakati kuwezesha wengine kutumia fursa hiyo.
Akizungumza na kina mama wa wilaya za Mkuranga, Bagamoyo na Rufiji, mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, alisema kukopa fedha na kutozirejesha ni kukwamisha jitihada za wengine ambao nao wanazitaka kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Mama Salma alisema kwamba, mtu anapokopa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi, ahakikishe anazitumia kwa kazi hiyo na sio vinginevyo."Kina mama wenzangu, mkopo ni mkopo, lengo lilokufanya uchukue mkopo ni mradi wa kujiletea maendeleo, usitumie fedha za mkopo kununua doti za khanga, huko ni kujisababishia matatizo bila sababu za msingi," alisema.Alifafanua kwamba, serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani ilikuwa na kauli mbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania, na fursa ya kupata mikopo, inalenga katika kuwezesha kauli mbiu hiyo kutekelezeka.Mama Salma aliwasisitizia wanawake kuendelea kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na VICOBA, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kupata fedha za mikopo kwa ajili ya kuendeleza na kuanzisha miradi ya uzalishaji mali.Kuhusu elimu, alisema mataifa yote yaliyoendelea, yamewekeza katika elimu ya watoto wao ndiyo maana serikali chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete katika miaka mitano yakuwepo madarakani, iliamua kujenga shule nyingi za sekondari na kupanua elimu ya vyuo na vyuo vikuu.Huku akiwaomba kina mama hao kumpigia kura mgombea urais wa CCM Rais Jakaya Kikwete na wagombea wa ubunge na udiwani wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu, Mama Salma alisema miaka ya sasa siyo ya kupuuzia elimu."Nchi yoyote yenye mafanikio imewekeza vyema katika elimu ya watoto wao, nasi hatuwezi kubaki nyuma katika hilo, shule nyingi tumejenga kwa nguvu zetu na msaada wa serikali, lakini pia tunakabiliwa na changamoto nyingi kuziwezesha kuwa bora zaidi," alisema."Mkikichagua tena Chama Cha Mapinduzi kitafanya kazi hiyo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi," alisema.

No comments:

Post a Comment