Friday, September 17, 2010

Ushirikiano ni nguzo muhimu

Misungwi

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewaambia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuwa, ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utapatikana iwapo watafanyakazi kwa ushirikiano.Alisema hayo juzi na jana alipozungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), katika wilaya za Geita, Sengerema, Kwimba na Misungwi, mkoani Mwanza.Mama Salma alisema kuna taarifa kwamba, baadhi ya maeneo viongozi wa CCM wapo katika ofisi moja lakini hawazungumzi wamenuniana kutokana na sababu mbalimbali.Alisema miongoni mwa sababu hizo ni matokeo ya kura za maoni za kuwapata wagombea wa udiwani na ubunge zilizopigwa Agosti 1, mwaka huu, ambapo baadhi ya viongozi waliwaunga mkono wagombea ambao walishindwa,hivyo kubaki na kinyongo."Kuna mahali katibu na mwenyekiti hawazungumzi, wamenuniana, kweli hapo kazi itafanyika?" Alihoji Mama Salma na kina mama kumuitikia kwa kusema "haifanyiki."Katika kuonyesha kuguswa na hilo, kina mama hao walikuwa wakikatisha hotuba ya Mama Salma kwa kusema "sema mama, waambie hao."Mama Salma alisema kwamba, ana uhakika CCM itashinda katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31,mwaka huu, lakini ushindi huo lazima uwe wa kishindo, na utapatikana kwa viongozi wa CCM na wanachama kuwa kitu kimoja katika mchakato wa kampeni hadi siku ya kupiga kura.Taarifa zilizowasilishwa kwake na makatibu wa UWT katika wilaya hizo, zilisema moja ya matatizo yaliyopo ni makundi miongoni mwa viongozi na wanachama yaliyosababishwa na matokeo ya kura za maoni.Mama Salma alissisitiza kwamba,  katika mchakato huo wa kura za maoni ilikuwa ni lazima wagombea kuwa na wanaowaunga mkono, kwani ingekuwa ni kituko kwa mtu kutangaza nia na kugombea asiwe na watu wanaomuunga mkono katika azma yake hiyo."Hivi wewe unaposema huyu hakuwa wangu, wakati chama kimeshateua mgombea, unamaanisha nini? Unafanya hivyo kwa masilahi ya nani? Tusifanye makosa, kwenye mambo ya msingi hatufanyi majaribio," alionya Mama Salma.Aliwaambia kina mama hao kwamba, wana kila sababu ya kujisikia fahari na Chama Cha Mapinduzi kwa namna serikali ilivyotekeleza yale yaliyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi.Miongoni mwa yaliyoahidiwa na kutekelezwa, ni ujenzi wa shule za sekondari, ujenzi wa barabara, na kwa wilaya hizo ni ununuzi na ukarabati wa vivuko vinavyofanya kazi ya usafirishaji wa abiria na bidhaa katika Ziwa Victoria.Mama Salma aliwanadi kwa kina mama hao, wagombea ubunge wa CCM, Dk. Charles Tizeba (Buchosa), Donald Max (Geita), Lorensia Bukwimba (Busanda), Richard Ndassa (Sumve) na Sharif Mansoor (Kwimba). Mbunge wa Sengerema ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja hana mpinzani.Mama Salma yuko katika ziara ya kuwatembelea wanachama wa UWT kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu na kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa mtindo maarufu wa 'mafiga matatu.'

No comments:

Post a Comment