Thursday, September 9, 2010

Anayependa maendeleo atatambua mafanikio ya serikali-Mama Salma

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amesema mtu anayependa maendeleo nchini, atatambua mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne. Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanawake wa wilaya za Kibaha, Chalinze na Bagamoyo, mkoani Pwani jana {24.8.2010}, alisema mengi yaliyoahidiwa na Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa 2005, yametekelezwa. Mama Salma Kikwete alisema, katika suala la maendeleo na mustakabali wa nchi, ni lazima wanawake waangalie ni chama gani chenye sera na ilani makini, katika kuwaletea maendeleo yao, na jamii yote ya Watanzania. Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho kuwa ni ujenzi wa shule za sekondari za kata, zilizoondoa tatizo la watoto wanaofaulu na kushindwa kuendelea sekondari kwa kukosa nafasi. Mama Salma alisema, ujenzi wa shule za sekondari umeongezeka kutoka 1,745 hadi 4,102 katika kipindi cha miaka mitano, jambo ambalo ni mafanikio makubwa, lakini kuna watu wanaojifanya kutoyaona. Kutokana na kuongezeka kwa shule hizo, alisema idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka ambapo uandikishaji wa kidato cha kwanza hadi cha nne ulitoka kuwa wanafunzi 401,598, mwaka 2005, hadi 1,401,559 mwaka 2009. Kuhusu miundombinu, alisema ujenzi wa barabara zinazounganisha mikoa na wilaya nchini umewezesha wananchi kusafiri kwa haraka kutoka sehemu moja ya nchi kwenda nyingine, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma. "Zamani ilikuwa kutoka hapa (Kibaha), hadi Lindi tulilazimika kulala njiani, lakini sasa mambo ni mazuri," alisema na kupigiwa kofi. Alisema, Chama Cha Mapinduzi kimetekeleza ilani yake kwa mafanikio makubwa, na asiye na macho haambiwi tazama, kwani wengine wanaona mafanikio hayo lakini wanajifanya hawaoni," alisema. Mama Salma aliwaomba kina mama hao kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu katika mtindo maarufu wa CCM wa mafiga matatu. "Siku ya tarehe 31 mwezi wa kumi, ukifika kituoni piga kura kwa mgombea urais wa CCM, mgombea ubunge wa CCM na mgombea udiwani wa CCM hayo ndiyo mafiga matatu," Alisema. Akizungumzia kura za maoni za CCM kuwapata wagombea ubunge na udiwani, Mwenyekiti wa WAMA alisema, zilisababisha makundi tofauti kwa sababu wagombea walikuwa ni wengi. Kwa vile mchakato huo umemalizika na wagombea kupatikana, aliwasihi wanachama wa CCM kuvunja makundi hayo na kuwa na kundi moja la CCM kwa ajili ya kukipatia Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao. Kesho, (Agosti 25, 2010) Mama Salma Kikwete ataendelea na ziara ya kuzungumza na wanawake katika wilaya za Kisarawe, Mkuranga na Rufiji, na Agosti 26, 2010 anatarajiwa kuwa Mafia.

No comments:

Post a Comment