Friday, October 8, 2010

Kigoma na Tabora

Mama Kikwete akipatiwa watoto mapacha yatima wa kiume na mama mlezi wa kituo cha kulelea yatima kilichopo kijiji cha Matyazo Kigoma.

Mama Salma Kikwete Oyeeee! wanawake wa kijiji cha Nguruka Kigoma Kusini wakimshangilia Mama Kikwete
 Jamani eee Kigoma neema ! hii ndio faida ya kilimo !wakulima wa kijiji cha Mtalima Kasulu.


 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimnadi Mgombea Ubunge Samuel Sitta.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimnadi mgombea (CCM)jimbo la Kigoma Mjini Peter Serukamba.

 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimia katika kijiji cha Mvugwe kiliopo halmashauri ya Kasulu (Kigoma) wakati akielekea Kigoma.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza katika mkutano wa ndani wa kampeni jimbo la Kasulu vijijini

Mama Kikwete akiwahutubia wanawake wa Kaliua (jimbo la Urambo Magharibi)Tabora katika mkutano wa ndani wa kampeni
 Mama Salma Kikwete akimnadi mgombea ubunge jimbo la Urambo Magharibi Prof. Juma Kapuya
 Mama Salma Kikwete akiwahutubia akina mama wa UWT Urambo Mashariki (Tabora)
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea shada la maua alipowasili Jimbo la Urambo Mkoani Tabora

Saturday, October 2, 2010

CCM inafanana na Mti wenye Matunda

Na Mwaandishi Maalum,Mtwara:
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amekifananisha Chama Cha Mapinduzi na mwembe ambao hurushiwa mawe kutokana na matunda yake. Alisema wapinzani wanaisema CCM kwa sababu serikali imefanya mambo mazuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa baada ya kutekeleza kwa mafanikio ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya 2005. “Ukiona wapinzani wanaisema sana CCM ujue imefanya mambo mazuri, ni sawa na mwembe wenye matunda hupigwa mawe, kwani umeshaona mwembe usio na matunda ukipigwa mawe,” alihoji. Mama Salma alisema hayo jana na juzi alipokuwa akizungumza kwa wakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika mkoa wa Mtwara. Kuhusu uchumi, aliwaambia uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni ukombozi kwa wakulima dhidi ya walanguzi. Taarifa iliyowasilishwa kwake ilieleza kwamba, uuzaji korosho kwa mfumo huo umewanufaisha wakulima ambao hulipwa malipo kwa awamu mbili hadi tatu kulingana na bei ya soko. Ilieleza kwamba, wakati serikali ya awamu ya nne inaiingia madarakani kilo moja ya korosho ilikuwa ikiuzwa kwa kati ya sh. 150 hadi 300, kwa sasa ni sh. 800 hadi sh.1000 kwa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani. Mama Salma alisema wanaoupinga mfumo huo, wanataka kuendelea kujitajirisha kwa jasho la wakulima kama ilivyokuwa huko nyuma. “Msidanayike, uuzaji wa mazao kwa stakakabadhi ya mazao ghalani ni ukombozi kwa wakulima, na serikali ya CCM inawapenda haiwezi kuwadhulumu ndiyo maana inasisitiza na kusimamia mazao kuuzwa kwa vyama vya ushirika,” alisema na kupigiwa kofi na vigelegele. Wakati akiwanadi wagombea ubunge Mariam Kasembe (Masasi), Jerome Bwanausi (Lulindi), George Mkuchika (Newala), Juma Njwayo (Tandahimba), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) na Mohamed Murji (Mtwara Mjini), Mama Salma alitoa wito kwa wanawake viongozi kupigania kwa dhati maendeleo ya kina mama wenzao. Alisema haipendezi mwanamke kiongozi kuwa kikwazo katika maendeleo ya wenzake, alibainisha Mama Salma na kushangiliwa na kina mama hao.

Sunday, September 26, 2010

Serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi ya 2005 kwa mafanikio makubwa.

Na Mwandishi Maalumu, Lindi
MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewataka wanachama wa CCM kutembea kifua mbele kwa sababu serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi ya 2005 kwa mafanikio makubwa.Alisema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti jana na juzi na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika majimbo ya Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini, Mchinga, Mtama, Lindi Mjini, Ruangwa na Nachingwea.Mwenyekiti huyo alisema kama yalivyo maeneo mengine nchini, ndivyo ilivyo katika majimbo hayo kwa maendeleo yaliyopatikana katika miaka mitano ya serikali ya awamu ya nne hali inayodhihirisha utekelezaji mzuri wa ilani hiyo.“Hivi mtu anapotoka huko na kusema CCM haijafanya lolote, alitaka ifanye nini? Wana-CCM tembeeni kwa kujidai kwa sababu katika kipindi cha miaka mitano serikali imefanya mambo mengi mazuri kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema na kupigiwa kofi.Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2005 katika majimbo hayo ilitaja baadhi ya maendeleo yaliyopatikana ni kuongezeka kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, kuboreka kwa barabara, huduma ya maji na kina mama kuwa na mwamko wa kujishughulisha na miradi inayowaingizia pesa.Mfano, katika wilaya ya Kilwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wamefikia 6,300 ikilinganishwa na 1,280 wa mwaka 2005, shule za sekondari zilikuwa nne kwa sasa ziko 25 huku idadi ya walimu ikiongezeka kutoka 35 na kufikia 128.Wilaya ya Kilwa kwa miaka mingi ilikuwa na tatizo sugu la upatikanaji wa umeme lakini kwa sasa shida hiyo ni historia baada ya kuwa na umeme wa uhakika unaotokana na gesi ya Songosongo.Mama Salma alisema, kwa mafanikio hayo ni wazi CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi, na kuwataka kina mama kutopoteza kura zao kwa kukivipigia kura vyama vya upinzani ambavyo haviwezi kushinda katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.Aliwataka wazazi kuwasimamia watoto wao wasome kwa bidiii kwa sababu elimu ndiyo msingi mkuu wa maendeleo kwa nchi yoyote.“Mtu asikudanganye, nchi zote zilizopiga hatua katika maendeleo zimewekeza katika elimu kwa vijana wao, na ndicho serikali imekifanya katika miaka mitano hii,” alisema.Alisema baada ya ujenzi wa shule za sekondari za kata kutia for a, ni dhamira ya Chama Cha Mapinduzi kuona wanaomaliza kidato cha nne wanaendelea kupata elimu ya kidato cha tano na sita, hivyo kila tarafa itajengwa shule yenye vidato hivyo.Alikemea tabia ya undumila inayoonyeshwa na baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM, akisema isipoachwa itakikosesha ushindi wa kishindo katika uchaguzi.“Wengine hapa mchana wamevaa kijani, usiku wako kwenye vyama vingine, kweli au si kweli,” alihoji Mama Salma na kujibiwa kwa sauti “kweli, sema mama.” Aliwasihi viongozi na wanachama waondoe tofauti miongoni mwao na kuwa kitu kimoja kuwezesha ushindi mkubwa kwa CCM, kwani kuendelea na hali ya kutofautiana ni kutoa upenyo kwa wapinzani.





Friday, September 17, 2010

Ushirikiano ni nguzo muhimu

Misungwi

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewaambia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuwa, ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utapatikana iwapo watafanyakazi kwa ushirikiano.Alisema hayo juzi na jana alipozungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), katika wilaya za Geita, Sengerema, Kwimba na Misungwi, mkoani Mwanza.Mama Salma alisema kuna taarifa kwamba, baadhi ya maeneo viongozi wa CCM wapo katika ofisi moja lakini hawazungumzi wamenuniana kutokana na sababu mbalimbali.Alisema miongoni mwa sababu hizo ni matokeo ya kura za maoni za kuwapata wagombea wa udiwani na ubunge zilizopigwa Agosti 1, mwaka huu, ambapo baadhi ya viongozi waliwaunga mkono wagombea ambao walishindwa,hivyo kubaki na kinyongo."Kuna mahali katibu na mwenyekiti hawazungumzi, wamenuniana, kweli hapo kazi itafanyika?" Alihoji Mama Salma na kina mama kumuitikia kwa kusema "haifanyiki."Katika kuonyesha kuguswa na hilo, kina mama hao walikuwa wakikatisha hotuba ya Mama Salma kwa kusema "sema mama, waambie hao."Mama Salma alisema kwamba, ana uhakika CCM itashinda katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31,mwaka huu, lakini ushindi huo lazima uwe wa kishindo, na utapatikana kwa viongozi wa CCM na wanachama kuwa kitu kimoja katika mchakato wa kampeni hadi siku ya kupiga kura.Taarifa zilizowasilishwa kwake na makatibu wa UWT katika wilaya hizo, zilisema moja ya matatizo yaliyopo ni makundi miongoni mwa viongozi na wanachama yaliyosababishwa na matokeo ya kura za maoni.Mama Salma alissisitiza kwamba,  katika mchakato huo wa kura za maoni ilikuwa ni lazima wagombea kuwa na wanaowaunga mkono, kwani ingekuwa ni kituko kwa mtu kutangaza nia na kugombea asiwe na watu wanaomuunga mkono katika azma yake hiyo."Hivi wewe unaposema huyu hakuwa wangu, wakati chama kimeshateua mgombea, unamaanisha nini? Unafanya hivyo kwa masilahi ya nani? Tusifanye makosa, kwenye mambo ya msingi hatufanyi majaribio," alionya Mama Salma.Aliwaambia kina mama hao kwamba, wana kila sababu ya kujisikia fahari na Chama Cha Mapinduzi kwa namna serikali ilivyotekeleza yale yaliyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi.Miongoni mwa yaliyoahidiwa na kutekelezwa, ni ujenzi wa shule za sekondari, ujenzi wa barabara, na kwa wilaya hizo ni ununuzi na ukarabati wa vivuko vinavyofanya kazi ya usafirishaji wa abiria na bidhaa katika Ziwa Victoria.Mama Salma aliwanadi kwa kina mama hao, wagombea ubunge wa CCM, Dk. Charles Tizeba (Buchosa), Donald Max (Geita), Lorensia Bukwimba (Busanda), Richard Ndassa (Sumve) na Sharif Mansoor (Kwimba). Mbunge wa Sengerema ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja hana mpinzani.Mama Salma yuko katika ziara ya kuwatembelea wanachama wa UWT kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu na kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa mtindo maarufu wa 'mafiga matatu.'

Wito kwa wagombea waliokosa wapinzani

NA MWANDISHI MAALUMU, KONGWA
 MWENYEKITI  wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao katika kata na majimbo yao wagombea wamepita bila kupingwa, wasibweteke, waendelee kufanya kampeni za nguvu kukiwezesha chama kupata  ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31, mwaka huu.Mama Salma alisema hayo Agosti 29, 2010,  alipozungumza na wanawake wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo.Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaomba kinamama hao kuwachagua wagombea wa CCM kwa mtindo maarufu wa chama hicho wa mafiga matatu, yaani diwani, mbunge na rais.Taarifa ya chama hicho wilayani Kongwa, ilieleza kwamba mbunge anayetetea nafasi yake katika jimbo la Kongwa, Job Ndugai wa CCM, amekosa mpinzani, na wagombea udiwani nane kati ya 22 nao wamepita bila kupingwa.Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa Kongwa kwa zaidi ya asilimia 85, ambapo kwa upande wa shule za sekondari zimeoongezeka kutoka tano mwaka 2005 hadi kufikia 24, huku baadhi ya kata zikiwa na shule tatu za sekondari kulingana na idadi ya wanafunzi wa maeneo husika.Kutokana na ongezeko la shule hiyo, taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Kongwa, Abdi Matali, ilisema wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari nao wameongezeka kutoka 1,324 mwaka 2005 hadi kufikia 9,850.Mama Salma alisema kwamba, CCM ina kila sababu ya kuchaguliwa kuendelea kushika dola kwa sababu imetekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 iliyonadiwa nchini kote na kukubaliwa na wananchi.

Monday, September 13, 2010

Mama Salma apongezwa kusaidia wanawake

 NA MWANDISHI MAALUMU, MUSOMA
WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Mara, wamempongeza Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, kwa jitihada zake za kushughulikia kero zinazowakabili wanawake pasipo kujali itikadi.Katika taarifa za utendaji kazi zilizowasilishwa kwake Septemba 13,2010, na makatibu wa UWT wa wilaya za Musoma Mjini, Musoma Vijijini na Bunda, mkoani humo, zilieleza kwamba Mama Salma amewasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi pamoja na kupigania elimu kwa watoto wa kike. Makatibu hao, Agness Methew (Bunda), Ashura Kimwaga (Musoma Mjini) na Hamisa Chacha (Musoma Vijijini), kwa nyakati tofauti walisema kwamba bila kujali itikadi amekuwa akiwawezesha kiuchumi kina mama katika vikundi vyao vya uzalishaji mali.
 Watendaji hao wa UWT walimsifu Mama Salma kwa kuwa mstari wa mbele kupigania elimu kwa watoto wa kike, jambo ambalo ni ukombozi katika maisha yao ya baadaye.Mama Salma ambaye yuko mkoani Mara kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu, na kuwapigia kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi, alisema kwamba, Ilani ya CCM ya 2005 ilizungumza kuwawezesha kina mama kiuchumi, na kuwapatia nafasi katika vyombo vya maamuzi, mambo ambayo yametekelezwa kwa kiwango kikubwa.Alifafanua kwamba uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake umefanyika kupitia vyama vya ushirika (SACCOS) hatua ambayo imewapa uwezo wa kumudu gharama za mahitaji yao na ya familia zao.Mama Salma aliwakumbusha kina mama hao kwamba, kwa kuwa fedha zinazotolewa kupitia SACCOS ni mikopo, ni muhimu kwa kila anayezikopa kuzirejesha kwa wakati kuwezesha wengine kutumia fursa hiyo na kujikwamua kiuchumi. “Licha ya wanawake kuwezeshwa kiuchumi katika kipindi hiki cha miaka mitano, pia wengi wapo katika ngazi za maamuzi,” alisema.Mama Salma aliwataka wanachama wa CCM kuyatangaza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2005 pasipo woga, kwa sababu mengi yaliyoahidiwa yametekelezwa kwa asilimia kubwa.Alifafanua kwamba, katika harakati za kuleta maendeleo, changamoto haziwezi kukosekana na kutoa mfano kwamba, mafanikio katika ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata nchini, yameibua upungufu wa walimu, maabara na nyumba za kuishi watumishi hao.Mama Salma alisema serikali inazifahamu changamoto hizo, na ndiyo msingi wa kuongeza bajeti ya elimu kuwezesha kutatuliwa na kuwepo kwa wanafunzi wengi wanaosomea ualimu katika vyuo mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo katika chuo chake cha ualimu, kila mwaka kitakuwa kikitoa wahitimu wa ualimu 15,000 hatua ambayo itaoondoa tatizo la watumishi hao nchini kote katika kipindi kifupi kijacho.Aliwasihi Watanzania wasidanganyike na kauli za wapinzani kwamba watakapoingia madarakani kila kitu kitakuwa bure, na hawatatoza kodi.“Hakuna serikali yoyote hapa duniani inayoendeshwa pasipo kutoza kodi. Tusidanganyike,” alisema na kuitikiwa; “hatutadanganyiki.” Mama Salma aliwanadi wagombea ubunge kupitia CCM, Stephen Wassira (Bunda) na Vedastus Mathayo (Musoma Mjini). Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono amepita bila kupingwa.Tayari Mama Salma ameshafanya ziara kama hiyo na kuzungumza na kina mama kwenye mikutano ya ndani, katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Singida, Manyara na Dar es Salaam.

Uhamasishaji wa ushiriki katika uchaguzi mkuu mkoani Mara

Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake (WAMA) Mama Salma Kikwete akisalimiana na Wanachama wa UWT Mkoa wa Mara Sept.12,2010 alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Musoma . Mama Salma Kikwete yupo mkoani hapo kwa ajili ya kukutana na wanachama wa UWT katika mikutano ya ndani kuhusu kuwahamasisha umuhimu wa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Ujao mwaka huu.(kulia) Mwenyekiti wa UWT mkoa Mara Nancy Sessani. (Picha na Mwanakombo Jumaa)














Chini;Katibu wa UWT Mara Helena Chacha akimkaribisha Mwenyekiti wa WAMA baada ya kuwasili Mkoani hapo kwa ziara ya kuwahamasisha ushiriki katika uchaguzi.














Mama Salma akifurahia ngoma ya asili wakati alipowasili Musoma 12,9,2010.